Endapo unahitaji kusafiri wakati pasi yako imeisha muda na uliyoomba haijaletwa Ubalozini au kama pasipoti imepotea, au unarudi nyumbani kwa sababu zozote zile na huna pasipoti, Ubalozi unaweza kutoa Pasi ya Dharura. Matumizi ya pasipoti ya dharura ni kwa safari ya kwenda Tanzania tu.

Ili kupata pasi ya dharura inatakiwa viambatanisho vifuatavyo;

  • Jaza Fomu za kuomba pasi ya dharura
  • Ambatanisha ushahidi wa Uraia wako wa Tanzania – Kitambulisho chochote kinachoonyesha kuwa wewe ni Mtanzania, cheti cha kuzaliwa etc.
  • Ripoti ya Polisi kuonyesha kuwa ulitoa taarifa ya kupotea kwa pasipoti (iwe kwa lugha ya kiingereza)
  • Nakala ya Pasipoti iliyopotea kama unayo
  • Barua ya kujieleza kwa nini unataka hati ya dharura
  • Picha 2 za pasipoti
  • Malipo ya SEK. 200 pamoja na SEK 90 kwa ajili ya kutuma kwa posta kama hukuja Ubalozini.

Mwombaji mwenye Pasi iliyopotea anatakiwa awe na ripoti ya polisi kwa lugha ya kiingereza. Awe na nakala ya pasi ya zamani au namba yake na DN namba toka pasi ya zamani ina saidia katika kupata kumbukumbu za mwombaji. Malipo kwa waliopoteza pasi ni SEK 1100.00. Maombi ya pasi mpya ni kama ilivyoelezwa hapo juu.

Ukihitaji kubadili jina kwa sababu yoyote ile kama ndoa inabidi uombe pasipoti mpya yenye jina jipya. Inabidi kuja Ubalozi kuomba. Andika barua ya kujieleza sababu ya kubadili na ambatanisha ushahidi wa kubadili aidha kwa ndoa au kwa kubadili kwa hiari uwe na hati (“deed poll”, cheti cha ndoa nk).

Barua iandikwe kwa Kamishana wa Uhamiaji, Dar es Salaam, K.K.K Ubalozi wa Tanzania Sweden.

Ubalozi wa Tanzania Stockholm kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji Dar es Salaam Tanzania wanajitahidi kuhakikisha kuwa Watanzania wanaoishi katika nchi za Nordic na Baltic ambao walituma maombi ya pasi mpya za kusafiria na bado hawajazipokea mpaka sasa wanapatiwa pasi hizo mapema iwezekanavyo.

Pasi nyingi zinazokawia kutolewa ni kwa sababu maombi yanaupungufu. Tafadhali tunaomba mzingatie masharti na viambatanisho vinavyotakiwa. Waombaji wanaohitaji kuambatanisha vyeti vya kuzaliwa, ndoa, barua ya polisi, kubadili jina n.k tunawaomba walete tafsiri zake kwa kiingereza. Wale wanaoahidi kutuma baada ya kuambiwa upungufu tunawaomba watekeleze haraka la sivyo maombi yao yanawekwa pembeni.

Ikiwa viambatanisho vyote vimekamilika na pasi bado imekawia msisite kutupigia Ubalozini Na. +46 8 7322430/31au kutuma barua pepe mkitumia anuani mailbox@tanemb.se. Katika taarifa hii tafadhali hakikisha unaleta:

  • Jina lako kamili
  • Eneo unaloishi/Anuani
  • Tarehe uliyoleta maombi yako

Ukipata taarifa hii tafadhali mweleze na mwingine

Pasipoti, hati nk. zinapoletwa Ubalozini toka Uhamiaji tunazitangaza hapa. Kwa watanzania walioko Stockholm wanakaribishwa kuchukua wao wenyewe hapa Ubalozini. Kwa wale walioko nje ya Stockholm wahusika wanaombwa watume anuani zao za sasa kwa barua pepe (mailbox@tanemb.se) ili tuweze kuwatumia kwa register. Kwa vile pasipoti ni muhimu ni vyema anuani ya muhusika anayotumia hivi sasa iandikwe kwa ufasaha ili kuzuia upotevu.

Wale ambao hawataona majina yao tunawaomba wawe na subira. Ikiwa utapatwa na dharura wakati ukisubiri pasi mpya, Ubalozi unaweza kutoa pasi ya dharura kwa safari ya kwenda Tanzania tu.