Taarifa Kutoka Kwa Balozi Kwenda Diaspora

Kwa Mwenyekiti TDC Global, Wenyeviti wa Vyama vya Watanzania katika nchi za Nordic, Baltic na Ukraine, na Watanzania wenzangu tulio Ughaibuni.

Salamu kwenu wote popote mlipo katika eneo lote la uwakilishi wa Ubalozi wetu.

Awali napenda kuwajulisha kuwa nilikuwa Dar-Es-Salaam na Msafara wa Wawekezaji na Wafanyibiashara kutoka baadhi ya nchi ninazoziwakilisha.

Napenda kuwajulisha kuwa tulikwenda na Makampuni 18, japo dakika za mwisho makampuni kadhaa yalijitoa kutokana na sera zao za ndani kuhusu hili “Janga” la kimataifa la virusi vya corona (COVID-19). Makampuni yaliyojitoa walituma mawakilishi wao wanaoishi Tanzania. Katika ujumla wake Kongamano la Mwaka huu lilifanikiwa kwa kiwango kikubwa. Tunachosubiri sasa ni kuona mahusiano ya kibiashara yatakayotokea baina ya Wawakezaji wa Kitanzania na wa Kiswidi, jambo ambalo ndilo lengo Kuu.

Nachukua nafasi hii kuwapa pole sana na janga hili linaloendelea. Kwa bahati nzuri sijasikia hadi sasa taarifa yeyote ya mtanzania mwenzetu aliyeathirika kwa namna yeyote ile. Tumeshuhudia hatua kali za udhibiti na kwa ujumla wageni waliridhika na hatua walizoziona pale uwanja wa Kimataifa wa Dar-Es-Salaam.

Ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kutulinda.

Napenda kuwaasa kila mmoja wetu achukue tahadhari kubwa kulinda maisha yake binafsi, na ya familia yake kwa kuzingatia maelekezo yote ya Serikali na Wataalamu wa Afya. Tujiepushe na mikusanyiko isiyo ya lazima, au safari zozote zisizo za lazima.
Tuepuke kukaribiana na kusalimiana kwa Taratibu za mila na desturi zetu ambazo kwa mujibu wa wataalamu ni hatarishi katika maambukizi ya virusi vya Corona (COVID-19).

Kipindi hiki sisi tulio ugenini tuonyeshe kwa karibu zaidi upendo wetu na kusaidiana kwa hali na mali. Tupeane taarifa zote muhimu na hasa pale moja wetu anavyoathirika kwa namna yeyote ile. Kupeana taarifa ni muhimu sana kwani kuwa ugenini peke yako na ugonjwa si ngumu, hivyo tukiweza kupeana faraja ni jambo jema, lakini bila kuharibu kanuni za kujikinga.

Nadhani mmekwisha soma kwenye tovuti yetu (web page) kuwa Ubalozi umesitisha huduma mbali mbali za kikonseli hasa zinazohitaji watu kufika ubalozini. Hii ni kwa sababu Ubalozi wenye umejiweka kwenye karantini kwa wiki mbili na tutaangalia hali itakavyokuwa.

Kimsingi, mimi nilivyotoka safari inatakiwa niwe karantini. Lakini pia mwenzetu aliyekutwa na virusi vya (COVID-19) alifika Sweden alitembelea pia ofisi za Ubalozi wetu hivyo tumetakiwa kuwa kwenye karantini japo hakuna mtu mwenye dalili yeyote ya virusi vya (COVID-19).

Napenda kusisitiza kuwa mawasiliano yetu yote yako wazi na msisite kututafuta moja kwa moja au kupitia namba zetu zilizoko kwenye tovuti yetu.

Nawashukuru sana na Mwenyezi Mungu awabariki sana.

Balozi Slaa,
Ubalozi wa Tanzania,
Stockholm, Uswidi
18.3.2020

Share This Post

More To Explore

Vice President Visit to Stockholm

The Vice-President Of The United Republic Of Tanzania, Dr. Philip Isdor Mpango Attends Stockholm+50′ Conference Read more…

Fursa Ya Uwekezaji Wa Nyumba Kwa Diaspora

Ubalozi unapenda kuwajulisha kuhusu fursa ya uwekezaji wa nyumba chini ya mradi uitwao Hamidu City Park uliopo Kigamboni jijini Dar es Salaam. Mradi huo unaomilikiwa na Bw. Hamidu Hemed Mvungi, una eneo lenye ukubwa wa ekari 140 ambalo lina nyumba 120 hivi sasa, zinazouzwa kwa gharama ya kuanzia Dola za Kimarekani 57,000 hadi 140,000. Kwa

Karibu Tanzania

The land of Kilimanjaro