MAOMBI YA PASIPOTI MPYA ZA KIELEKTRONIKI KUPITIA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI SWEDEN.

Watanzania waishio katika eneo la uwakilishi wa Ubalozi wa Tanzania katima nchi za Nordic na Baltic wanakaribishwa kuomba pasi halisi mpya na pasi ya dharura kwa kujaza fomu kwa njia ya mtandao inayopatikana katika Tovuti rasmi ya Idara ya Uhamiaji (www.immigration.go.tz) sehemu ya e-services utakuta fomu ya maombi ya Pasipoti (Passport application fomu). 

Tuzingatie kuwa ujazaji wa fomu haufanyikii Ubalozini isipokuwa tunapokea fomu zilizojazwa kwa mtandano na kupakuliwa na mwombaji mwenyewe kabla ya kupangiwa miadi ya kuja Ubalozini kwa hatua zinazofuata.

Vile vile, kila mwombaji ahakikishe anazo nyaraka zote muhimu na kuziingiza kadiri mfumo utakavyoelekeza vinginevyo ombi husika haliwezi kufanyiwa kazi. Nyaraka zinazohitajika ni kama ifuatavyo: –

  1. Cheti cha Kuzaliwa cha Mwombaji au Hati ya Kiapo (Affidavit) kwa wasio na Cheti cha kuzaliwa (kwa waliozaliwa Tanzania). Waliozaliwa Nordic na Baltic kama hawana cheti cha kuzaliwa, taarifa ya mwombaji toka “Population Registry” inaweza kuambatanishwa pamoja na cheti cha kuzaliwa mzazi Mtanzania.
  2. Cheti cha Kuzaliwa cha Mzazi mmoja (Baba au Mama) wa Mwombaji au Hati ya Kiapo (Affidavit) kwa Wazazi wasio na cheti cha kuzaliwa. Ifahamike kwamba Cheti cha kuzaliwa au Affidavit ya Mzazi mmoja ni hitajio la lazima hata kama wazazi wamefariki. Affidavit zitengenezwe Tanzania.
  3. Picha moja ya Pasipoti (yoyote ila ukija Ubalozini utapigwa nzuri yakutengenezea pasi)
  4. Kitambulisho cha Taifa (Lakini sio lazima kama huna)
  5. Nakala ya Kitambulisho cha ukaazi (Residence permit) cha nchi unayoishi kinachothibitisha kuwa mwombaji ni raia wa Tanzania
  6. Nakala ya Pasipoti ya zamani.

Baada ya mwombaji kukamilisha kujaza fomu mtandaoni atalipia $ 90 kwa njia ya mtandao wa malipo ya serikali (https://epay.gepg.go.tz) na kisha kuchapisha (Print) fomu yake na kuomba miadi kwa kupiga simu (+4687322430) au kutuma barua pepe (consular@tanemb.se) Ubalozini ili kupangiwa siku na muda wa kuja kukabidhi fomu zake kwa afisa wa Pasipoti Ubalozini kwa hatua zaidi.

Afisa wa Pasipoti akishapokea fomu na kuhakiki usahihi wa taarifa zilizojazwa kwa mujibu wa nyaraka zilizoambatanishwa na kuridhika, mwombaji ataingia kwenye hatua ya kupiga picha, Alama za vidole na kuweka saini.

Baada ya hatua za hapo juu kukamilika, maombi yatatumwa Uhamiaji kwa ajili ya kufanyiwa kazi.